YALIYOJIRI KATIKA SEMINA YA MATUMIZI SAHIHI YA VIPIMO WILAYA YA CHAMWINO DODOMA TAREHE 16.11.2023

Imewekwa:November 16, 2023

Mkuu wa Wilaya ya Chamwino Mhe. Gift Msuya amewaasa Madiwani wa Halmashauri hiyo kuwahimiza Wananchi kutumia Vipimo sahihi katika Biashara na katika ufungashaji wa mazao ya kilimo pia.

Mkuu wa Wilaya amesema hayo katika kikao kilichoandaliwa na Wakala wa Vipimo Mkoa wa Dodoma kwa lengo la kutoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya Vipimo.

Kadhalika, Mkuu wa Wilaya amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kuhakikisha mizani za kupimia uzito wa wanyama zinanunuliwa na kufungwa ili mauziano ya mifugo yafanyike kwa kuzingatia uzito ili mfugaji asipunjike.

Mkuu wa Wilaya pia amezitaka Halmashauri kuanzisha vituo vya mauzo ya mazao ambavyo vitakuwa na mizani iliyohakikiwa ili kuwalinda Wakulima wasipunjike kupitia udanganyifu wa Vipimo.

Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa Vipimo Mkoa wa Dodoma Bw. Karimu Zuberi ameeleza kuwa elimu inayotolewa kwa Waheshimiwa Madiwani ni endelevu ambapo ilianza katika Wilaya za Mpwapwa, Dodoma Manispaa na Kongwa na lengo ni kuwapa uelewa wa elimu ya Vipimo ili waweze kuwaelekeza Wananchi katika maeneo yao.

Vilevile, Diwani wa kata ya Mlowa barabarani Mhe. Angelo Lukas ameipongeza Wakala wa Vipimo Mkoa wa Dodoma kwa elimu nzuri ambayo itawasaidia kuwapa elimu Wananchi katika maeneo yao kwa kuwa Vipimo ni sehemu ya Maisha ya kila siku ya mwanadamu.

Ameeleza kuwa hivi karibuni Wakala wa Vipimo ilikuwa katika kata yake kwa ajili ya kuhakiki Vipimo na Wananchi wamefurahi sana kwakuwa sasa wananunua bidhaa bila kupunjika kwakuwa awali malalamiko yalikuwa mengi kuhusu Vipimo madukani.


IMEANDALIWA NA SEHEMU YA MAWASILIANO NA UHUSIANO KWA UMMA WMA