YALIYOJIRI KWENYE KIKAO CHA MENEJIMENTI CHA TATHMINI YA UTENDAJI WA WAKALA WA VIPIMO
Imewekwa:July 21, 2023
Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt. Hashil Abdallah amewataka viongozi wa Wakala wa Vipimo kujikita zaidi kwenye kusaidia uwezeshaji kwenye Biashara kwa kuhakikisha inatoa elimu ya kutosha kuhusu umuhimu wa kutumia Vipimo na kuhakikisha wafanyabiashara wanazalisha bidhaa zenye Vipimo sahihi .
Dkt.Hashil ameyasema hayo leo 21Julai,2023 wakati wa akifungua kikao cha menejimenti ya Wakala ambacho kinafanyika kwenye shule ya uongozi ya Mwalimu Nyerere Kibaha Mkoa wa Pwani.
Kadhalika, Dkt. Hashil amewataka mameneja hao wa mikoa yote ya kivipimo Tanzania Bara kutekeleza majukumu yao kwa ufasaha na ufanisi zaidi kwakuwa majukumu wanayofanya wanatekeleza kwa niaba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Pamoja na mambo mengine amehimiza viongozi kujikita kutatua changamoto na kupunguza malalamiko yanayoweza kujitokeza na ameahidi kuendelea kufuatilia kwa ukaribu utendaji kazi wa Wakala ili kuhakikisha maelekezo mbalimbali anayotoa yanafanyiwa kazi ili kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi,amesisitiza pia kuwa katika mikoa 30 ya kivipimo ni mikoa 6 ambayo hajaifikia na ataifikia ili kufuatilia utendaji kazi wake.
Wakati huohuo,Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo Bi. Stella Kahwa amesema kupitia kikao hiki ni muhimu kukumbushana na kujinoa na kutekeleza kwa usahihi shughuli za wakala kwani kwani vikao hivi vya tathmini vinasaidia kuona malengo na kubaini changamoto zinatatuliwaje.
Wakala wa vipimo umekuwa ukifanya vikao hivi kila robo mwaka kwa nia ya kutathimini utendaji kazi na kupanga mipango ya utekelezaji wa majukumu yake.
IMEANDALIWA NA SEHEMU YA MAWASILIANO NA UHUSIANO KWA UMMA