YALIYOJIRI WAKATI WA MKUTANO WA WMA NA WAANDISHI WA HABARI KWENYE UKUMBI WA HABARI MAELEZO DODOMA

Imewekwa:August 15, 2023

YALIYOJIRI LEO WAKATI WA MKUTANO WA WAKALA WA VIPIMO NA WAANDISHI WA HABARI KWENYE UKUMBI WA HABARI MAELEZO DODOMA TAREHE 15/8/2023

Wakala wa Vipimo katika utekelezaji wa majukumu yake unasaidia katika kujenga uchumi wa kisasa, shirikishi na shindani, msingi mkuu wa kufanikisha haya ni kuwa na viwanda vinavyotumia ipasavyo vilivyohakikiwa na kukidhi matakwa ya kimataifa (Traceability to International Standards) ambavyo huongeza tija, ufanisi na usahihi wa vipimo vya bidhaa zinazozalishwa kwenye viwanda hivyo kuwa shindani katika soko la ndani na la nje matokeo yake ni kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi na pato la Taifa.

Wakala wa Vipimo katika utekelezaji wa majukumu yake imeendelea kutoa mchango katika kuchochea maendeleo ya sekta za kiuchumi na kijamii nchini, kuchochea uzalishaji wa bidhaa unaozingatia vipimoti sahihi, kuendelea kuchangia katika mfuko mkuu wa Serikali.

Katika kuhakikisha Kilimo kinaendelea kuwa nguzo muhimu katika kuchochea uchumi wa nchi, Wakala wa Vipimo imeendelea kufanya uhakiki wa vipimo vinavyotumika katika kilimo ambavyo kwa sehemu kubwa ni mizani. Kwa mfano katika mazao ya kimkakati katika kipindi cha mwaka 2022/23 wakala ilihakiki jumla ya mizani 4254 (Pamba 1566, Korosho 2286 na Kahawa 402).

Vipimo hivyo vyote nilivyovitaja, ndivyo vinavyotumika kwenye hatua mbalimbali za kilimo mfano kuandaa eneo la kulima ni lazima ujue ukubwa wa eneo kwa kutumia vipimo vya urefu, kujua kiasi cha Mbolea itakayotumika kwa kupima kwa mzani au vipimo vya ujazo.

Ili kuleta ufanisi katika zoezi hili, elimu hutolewa juu ya umuhimu wa kufanya uhakiki wa Mizani inayotarajiwa kutumika katika kufanya ununuzi wa mazao kwa kushirikiana na vyama vya ushirika vya msingi, Sekretariati za Mikoa na baadae kufuatiwa na zoezi la uhakiki na baadaye kufuatiwa na kaguzi za kustukiza wakati ununuzi wa mazao unaendelea ili kubaini watumiaji wa mizani wasiozingatia matumizi sahihi ya vipimo, taratibu na Sheria.

Ili kuchangia katika kuleta mageuzi ya kilimo, na kuwa na uhakika wa chakula na hatimaye kujitegemea kwa chakula wakati wote ili kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya uchumi matumizi ya Vipimo vilivyohakikiwa kupitia Wakala wa Vipimo ni muhimu sana.

Mafuta na Gesi

Katika sekta hii hadi sasa kwa upande wa mafuta; Wakala wa Vipimo inafanya uhakiki wa vipimo vinavyotumika kuhifadhia, kusafirishi na kuuzia kiasi cha Mafuta kwenye maeneo mbali mbali kama vile kwenye meli zinazoleta Mafuta hapa nchini, kwenye maghala ya kuhifadhia Mafuta, na kwenye vituo vya Mafuta kwa wateja wa reja reja.

Uhakiki huu wa vipimo katika maeneo hayo yote hufanyika kwa lengo la kulinda pande mbili zinazofanya biashara hiyo kwa wakati husika. Mfanu: Meli iletayo mafuta hapa nchini inahusisha muuzaji na muagizaji au mnunuzi wa Mafuta hayo hivyo basi Wakala wa Vipimo huhakikisha vipimo vinavyotumika katika makabidhiano ya bidhaa hiyo vimehakikiwa ili kuhakikisha haki na usawa baina ya pande husika.

Tenki za kuhifadhia mafuta baada ya kutoka melini nazo pia hufanyiwa uhakiki kufahamu ujazo wa tenki ili kuhakikisha kuwa kiasi sahihi cha mafuta yaliyotoka melini ndio yaliyofika kwenye tenki husika kwa ajili ya kuhifadhiwa na kusubiri kusambazwa kwenye maeneo mbalimbali.

Dira zitumikazo kupimia kiasi cha mafuta yaliyopita kutoka melini kwenda kwenye tenki za kwenye maghala na mita zitumikazo kupima kiasi cha mafuta tenki kwenye tenki za kwenye maghala kwenda kwenye tenki za magari yakusafirishia mafuta nazo huhakikiwa na Wakala wa Vipimo ili kuhakikisha kiasi sahihi cha mafuta kinachotolewa wakati huo,

Tenki za magari yanayotumika kusafirishia mafuta ndani na nje ya nchi hufanyiwa uhakiki ili kuwa na uhakiki wa kiasi cha mafuta kinachosafirishwa kwa wakati huo lakini pia kumuwezesha dereva kuwa na uhakiki wa kiasi cha mafuta aliyokabidhia kwa ajili ya kusafirisha; Mwisho, tenki za kuhifadhia Mafuta na Pampu zinazotumika kuuzia mafuta kwenye vituo vya mauzo kwa rejareja.

Kwa upande wa sekta ya Gesi, Wakala wa Vipimo inasimamia kiasi cha gesi inayoingia hapa nchini kwa meli zitokazo nje ya nchi ili kujua kiasi cha gesi hiyo (LPG) iliyoagizwa na wafanyabiashara wetu hapa nchini ili kujiridhisha kuwa wanunuzi wa bidhaa hiyo hapa nchini wanapata kiasi sahihi kulingana na thamani ya fedha iliyolipwa.

Wakala wa Vipimo hufanywa ukaguzi na uhakiki wa mitungi ya gesi ya ujazo tofauti tofauti ili kuhakikisha kuwa wanunuzi wa gesi hiyo ya kupikia majumbani wanapata kiasi sahihi kulingana na thamani ya fedha waliyolipa.

Maji

Katika sekta ya maji Wakala wa Vipimo kwa sasa inafanya uhakiki wa Dira zote za Maji zinazotumiwa na Mamlaka za maji kufunga kwa wateja wao. Uhakiki unafanywa kwa dira zote mpya na zile ambazo tayari zipo katika matumizi ili kuhakikisha Mamlaka za maji zinapata tozo sahihi kwa maji yaliyotumiwa na mteja na mteja nae analipa gharama sahihi kulingana na maji aliyoyatumia.

Uhakiki wa dira hizi ni sehemu ya mambo ya msingi yanayochangia katika utekelezaji wa Ilani ya Chama Tawala kwa kuhakikisha huduma ya majisafi na salama inaendelea kuimarishwa na kuwafikia zaidi ya asilimia 85 ya wakazi wa vijijini na zaidi ya asilimia 95 kwa mijini ifikapo mwaka 2025.

Uhakiki wa dira za maji ulianza rasmi mwezi Machi, 2019 na maker kufikia June, 2023 Wakala imefanikiwa kuhakiki jumla ya dira za maji 420,497 kutoka kwenye Mamlaka mbalimbali za maji nchini.

Usafiri - Barabara, Majini na Angani

Katika sekta ya Usafiri kwa njia ya Barabara, Wakala wa Vipimo imeendelea kushirikiana na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) ili kuhakikisha Mizani zinazotumika kupimia uzito wa magari yapitayo kwenye Barabara hizo zisiharibike mapema.

Kwa upande wa Usafiri wa anga, Wakala wa vipimo imeendelea kuhakiki Mizani yote inayotumika kwenye viwanja vya ndege ili kuwa na uhakiki wa kiasi cha uzito unaobebwa kwenye ndege husika ili kuepusha ndege hizo kupata ajali kutokana na kubeba uzito mkubwa, Pamoja na Mizani hiyo ya kwenye viwanja vya ndege, Wakala imeendelea kuhakiki mita za tenki na mita za mafuta zinazotumika kuweka mafuta kwenye ndege ili kuhakikisha mafuta yanawekwa kwenye ndege hizo ni sahihi kulingana na uwezo wa ndege husika.

Kwa upande wa Usafiri wa majini, Wakala wa Vipimo imeendelea kuhakiki Mizani na vipimo vya ujazo vinavyotumika kupakilia Mizigo au Mafuta kwenye vyombo hivyo vya Usafiri ili kuwa na uhakiki na uzito au ujazo sahihi uliobebwa na chombo hicho ili kuepusha ajali ambazo zinaweza kutokea kutokana na kuzidisha uzito.

Umeme

Katika kuendeleza jitihada za Serikali kusambaza umeme mijini na vijijini ambapo jumla ya vijiji 8,587 kati ya vijiji 12,319 vya Tanzania Bara vimefikiwa na umeme ambayo ni sawa na asilimia 70; Wakala wa Vipimo imejipanga kufanya uhakiki wa mita zitakazokuwa zikifungwa kwa wateja wanaopokea umeme huo ili kuhakikisha Serikali inapata tozo iliyo sahihi kulingana na umeme uliosambazwa na mteja alipa kiasi sahihi kulingana na kiasi cha umeme aliipokea.

Madini

Sekta ya madini ni sekta muhimu kutokana na kuchangia kwake katika mapato ya Serikali na kutoa ajira kwa Watanzania, hususan katika ngazi ya wananchi wa kawaida. Serikali imeinunulia WAKALA vipimo vya kisasa vya uhakiki wa mizani inayotumika kupima vito na madini ili kuhakikisha upimaji wa madini unafanyika kwa usahihi.

Wakala uhakiki mizani inayotumika kupima madini katika masoko ya madini kabla haijaanza kutumukika na kufuatilia mwenenendo wake wakati wa matumizi. Matumizi ya vipimo sahihi huwezesha upatikanaji wa takwimu sahihi hivyo huwezesha upatikanaji wa pato sahihi la Serikali.

Ufugaji

Sekta ya mifugo ni miongoni mwa sekta muhimu katika ukuaji wa uchumi. Kutokana na umuhimu huo, ni dhahiri kuwa ipo haja ya kuendelea kuimarisha ufugaji wa kisasa na kuchakata/kusarifu bidhaa za mifugo kwa ajili ya mahitaji ya ndani, ikiwemo ya lishe bora, na usafirishaji nje.

Ili kuendeleza kutoa mchango kwenye sekta hii, Wakala imeendelea kutoa elimu juu ya umuhimu wa matumizi ya vipimo sahihi katika kufanya malisho ya Wanyama, uuzaji wa Wanyama kwa uzito pamoja malighafi kama mbolea.

Katika kufanikisha lengo hilo, mwezi Februari, 2023, Wakala wa Vipimo imeendelea kuhakiki Mizani inayotumika kwenye minada ya kuuzia Wanyama na mwezi Feb, 2023 Wakala ilihakiki Mizani 84 iliyonunuliwa na TAMISEMI kwa ajili ya kusambazwa kwenye minada mbali mbali ya mauzo ya Wanyama ili kuhakikisha Wanyama wanauzwa kwa uzito na sio kwa muonekano

Uchangiaji wa Wakala wa Vipimo katika mfuko mkuu wa Serikali

Katika kuonyesha manufaa ya kuanzishwa kwa Wakala wa Vipimo kwa lengo la Kupunguza gharama za uendeshaji na kusaidia maeneo mengine ya huduma za kijamii ambayo ya umuhimu na uhitaji mkubwa, Wakala wa Vipimo imeweza kuchangia jumla ya shilingi billioni 24,369,081,142.89 katika muda wa miaka mitano kuanzia mwaka 2018/19 hadi 2022/2023 kwa mchanganuo ufuatao: -

2018/2019 (4,044,160,480.68), 2019/2020 (5,328,909,792.12), 2020/2021 (6,414,274,906.93), 2021/2022 (4,183,490,575.20), 2022/2023 (4,398,245,387.96) Jumla 24,369,081,142.89

Uboreshaji wa Mazingira ya Utendaji Kazi na Utoaji Huduma

Katika kuendelea kuboresha Mazingira ya utendaji kazi kwa watumishi wa Wakala wa Vipimo, Wakala wa Vipimo ina ofisi katika Mikoa yote Tanzania Bara na imeainisha vituo vya muda vya uhakiki vipatavyo 5030 kwa ajili ya kusogeza huduma ambapo maafisa huweka vituo vya muda kwa ajili ya uhakiki. Huduma zetu hutolewa kwa mteja kuleta kipimo chake katika ofisi zetu, au kwa wakaguzi kwenda kukagua kipimo kwa mteja au mteja kuleta kipimo katika vituo maalumu vya muda.

Kwa sasa Wakala wa Vipimo imeendelea kuimarisha mazingira ya utendaji kazi kwa kuboresha ofisi za wakala katika mikoa mbalimbali, kuongeza vitendea kazi na mafunzo kwa watumishi. Aidha kwa sasa, Wakala wa Vipimo ina jenga jengo la ghorofa nne katika eneo la medeli hapa katika jiji la Dodoma ambalo ndilo litatumika Makao Makuu ya Wakala wa Vipimo. Ujenzi wa jengo hili kwa sasa umefikia zaidi ya asilimia 65 na linatarajiwa kukamilika mnamo Dec, 2024.

Ununuzi wa Vifaa vya Kitaalam

Ili kutoa huduma isiyo na mashaka katika uhakiki wa vipimo, Wakala wa Vipimo imeendelea kununua vifaa vya kitaalam ili kuhakiki vipimo na matokeo ya upimaji huo yasiwe na mashaka katika wigo wa Viwango vinavyokubalika kimataifa.

Katika kipindi cha miaka mitano baadhi ya vifaa vya kitalaam vilivyonunuliwa na Wakala wa Vipimo ni mitambo mitatu ya kuhakikia mita za Umeme, Mtambo mmoja wa kisasa wa kuhakikia mita za maji, mitambo saidizi kumi na tano (15) ya kufanyia uhakiki wa mita, mitambo 12 ya kuhakikia mita za maji zitumikazo majumbani.

Ununuzi wa vifaa hivi vya kitaalam umesaidia sana Wakala wa Vipimo kuongeza idadi ya vipimo vinavyohakikiwa kila mwaka ikiwemo kuingia kwenye maeneo mapya yanayohitaji huduma ya uhakiki wa vipimo Kipindi 2018/19, 2019/20, 2020/21, 2021/22, 2022/23 Vipimo (745,702) (837,306) (841,603)

(975,175) (986,342).

Wakala wa Vipimo inaahidi kuendelea kutekeleza majukumu yake kwa Weledi na ufanisi kwa kuendelea kusimamia Sheria ya Vipimo sura 340 kwa kusaidia na kufanya kazi sambasamba na wadau wa sekta mbalimbali kama vile Mafuta, Madini, Usafirishaji, Kilimo ili kuhakikisha sekta zote zinakuwa na mchango mkubwa kwenye kuongeza pato la Taifa na ukuaji wa uchumi.

Wakala wa Vipimo itaendelea kushiriki kikamilifu katika kushiriki kukamilisha miradi ya kimkatati kama vile Ujenzi wa Reli ya Kisasa kwa Kiwango cha Kimataifa (Standard Gauge Railway- SGR) na mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (Megawati 2,115) kwa kuhakikisha vipimo vinavyotumika katika maeneo hayo vimehakikiwa kwa mujibu wa Sheria ya Vipimo, baadhi ya Vipimo hivyo ni Malori yabebayo Mchanga, Kokoto na Vifusi, Mizani ya daraja (Weighbridges) pamoja na mita na Pampu zinazotumika kuwekea mafuta kwenye mitambo iliyopo katika miradi hiyo.

Kadhalika, katika kuendelea kuboresha na kufikisha huduma bora kwa wananchi Wakala wa Vipimo imeanza kutumia Mfumo wa Huduma za Serikali kupitia Simu za Mkononi (mGov). Mfumo huu umetengenezwa kwa lengo la kujumuisha huduma zote za simu za mkononi Serikalini. Mfumo huu unatumia sms katika kutoa na kupokea taarifa. Taarifa zinazopatikana katika mfumo huu zinaweza kutoka serikalini kwenda kwa wananchi au kutoka kwa wananchi kwenda serikalini kupitia namba 15200.

Wakala wa Vipimo inatoa wito kuwa, wananchi waendelee kujifunza kwa kupata elimu kuhusiana na matakwa ya sheria ya vipimo sura 340 ili kujikinga na matumizi yasiyofaa ya vipimo kwa baadhi ya watumiaji wasio waaminifu.