Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Viwanda na Biashara
Wakala wa Vipimo
Vipimo Sahihi na Vya Kuaminika kwa Wote
Background

Habari

WAFANYABIASHARA JIJINI DAR ES SALAAM WAHIMIZWA KUTUMIA VIPIMO SAHIHI

Imechapishwa na Paulus Olochi May 19, 2026

Wito umetolewa kwa wafanyabiashara jijini Dar es Salaam kuacha mara moja tabia ya udanganyifu wa kuchezea vipimo na kutumia vipimo visivyo sahihi kama vile 'lumbesa'. Serikali imesisitiza kuwa matumizi ya vipimo sahihi ni suala la kisheria na kimaadili, na badala yake imewataka wafanyabiashara kuunga mkono juhudi za kuwalinda walaji kwa kutumia vipimo sahihi.


Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, ametoa wito huo tarehe 18 Mei, 2026 katika Soko la Kariakoo wakati akizungumza na wafanyabiashara na viongozi wa masoko jijini humo, akisisitiza umuhimu wa kuzingatia matumizi sahihi ya vipimo na kutenda haki katika biashara wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kutokomeza matumizi ya vipimo batili ikiwa ni kuelekea katika Maadhimisho ya Siku ya Vipimo Duniani yanayofanyika tarehe 20 Mei Jijini Dodoma.


Chalamila alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haikusudii kuwa adui wa wafanyabiashara, bali inathamini mchango wao katika kukuza uchumi. Hata hivyo, alionya kuwa mafanikio hayo hayapaswi kujengwa juu ya misingi ya udanganyifu.


Katika hotuba yake, Mkuu wa Mkoa aliwakumbusha wafanyabiashara hao kuwa wajibu wa kupima kwa usahihi umeelezwa wazi katika vitabu vitakatifu vya dini zote mbili (Quran na Biblia), na kuongeza kuwa matumizi ya mizani na vipimo vilivyohakikiwa na Wakala wa Vipimo (WMA) ni ya lazima na si ya hiari.


"Mwananchi anapokwenda sokoni kununua bidhaa anatarajia kupata kiasi sahihi cha bidhaa. Anapopata pungufu kwa sababu ya vipimo batili kama makopo, visado au lumbesa, tunapoteza uaminifu wake," alisema Chalamila.

Aidha, aliwataka viongozi wa masoko kusimama kama walinzi wa kwanza kwa kuhakikisha hakuna vipimo batili vinavyotumika katika maeneo yao. Aliwaasa wafanyabiashara kuwa mabalozi wa vipimo sahihi na kutoa taarifa pale wanapobaini uwepo wa udanganyifu.

 

Kadharika, katika uzinduzi wa kampeni ya kutokomeza matumizi ya vipimo batili Mkuu wa mkoa amegawa tuzo iliyotolewa na Wakala wa Vipimo kwenda kwa viongozi wa Soko la Kisutu kwa kulitambua kama soko la mfano na kinanara katika matumizi ya vipimo sahihi jijini Dar es Salaam.

Pia, Mkuu wa Mkoa amegawa mizani mikubwa ya kilogramu 150 kwa viongozi wa masoko ya Ilala, Stereo Temeke, Machinga Complex, soko la mabibo pamoja na soko la Kariakoo ambalo limeongezewa mizani 20 ya kielektroniki ya kilogramu 40 kwa ajili ya kugawa kwa wafanyabiashara wa soko hilo.


Naye Mkurugenzi wa Ufundi Wakala wa Vipimo Bw. Francis Olwero amemuhakikishia Mhe. Albert Chalamila kuwa Wakala itaendelea kutoa elimu kuhusu umuhimu wa kutumia vipimo sahihi katika biashara pamoja na kuendelea kufanya ukaguzi wa kisheria na kaguzi za mara kwa mara za kushtukiza katika masoko yote na hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mtu yeyote atakayebainika kutumia vipimo kinyume na sheria ya Vipimo.

Mhe. Albert Chalamila amesisitiza wananchi wote wa Jiji la Dar es Salaam kuendelea kujielimisha kuhusu haki zao za msingi za kupimiwa bidhaa kwa usahihi, hatua ambayo itajenga uchumi wenye uwazi, haki na ushindani thabiti wa kibiashara

 


Widget Logo